Monday 7 July 2014

On 23:31 by Unknown   No comments
WAGANGA na wakunga wa tiba asili ni miongoni mwa watoa huduma za afya
 mbadala nchini ambapo wanaongozwa na sheria, mila, desturi na taratibu 
za tiba zilizopo nchini. 
 
   
moja ya vitu vinavopigwa vita na watabibu wa asili. 
  
    Kama ilivyo kwa mikoa mingine nchini, Mkoa wa Mbeya una idadi kubwa 
ya waganga wa tiba asili (pamoja waganga wa jadi/kienyeji) wanaokadiriwa
 kufikia 3261. Hata hivyo, uchunguzi unaonesha kwamba wengi kati ya 
waganga hao hawajasajiliwa kwa mujibu wa Sheria namba 23 ya mwaka 2002 
ya Tiba za Asilia na Tiba Mbadala na hivyo wanaendesha shughuli zao 
kinyume cha taratibu
Uwepo wa idadi kubwa ya waganga kiasi hicho ni kuonesha kwamba 
wananchi wengi bado wana imani na tiba ya asili japo watoa huduma hiyo 
wanafanya shughuli zao bila kufuata sheria inayowataka wasajiliwe. 
Tanzania ni moja ya nchi zilizoridhia kuwepo kwa Siku ya Tiba Asili ya 
Mwafrika baada ya mawaziri wa afya wa nchi 46 barani Afrika ambao pia ni
 wanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika, kuridhia 
kuwepo kwa sherehe hizo.
 Nia ni kufufua ari na kujenga heshima ya huduma ya Tiba ya Asili 
lakini mkazo ukiwa ni kutoa huduma sahihi. Historia inaonesha kwamba 
tiba za asili zimekuwepo kwa muda mrefu, zimekuwa zikiandikwa kwa maana 
ya kuonesha umuhimu wake na wakati mwingine kuonesha ubaya wake na hivyo
 kudharaulika.
Bado jamii zinazoishi maporini zinajitibu kwa kutumia tiba hizi 
asili. Kwa kiwango kikubwa, ukoloni mkongwe, ukoloni mamboleo na 
maendeleo ya sayansi na teknolojia, vinatajwa kuwa mpinzani mkuwa wa 
tiba za asili ya Mwafrika na kufanya baadhi ya watu kuzinyanyapaa tiba 
hizo hata pale zinapoonesha uwezo.
Pamoja na kwamba kuna matapeli wengi katika tiba hizi na pamoja na 
ukweli kwamba zimekuwa pia msaada wa magonjwa mengi kwa wananchi, 
kubezwa kwake kumefanya ‘wataalamu’ wengi wa tiba asili wayumbe, wakose 
dira na mwelekeo, mintarafu suala zima la kuboresha tiba asili nchini.
   Hii inaelezwa ni tofauti na nchi kama China na India ambapo tiba 
asili kwa maana ya mitishamba imekuwa ikifanyiwa kazi, kuchunguzwa 
kitaalamu na kuwekwa katika mfumo wa kisasa wa vidonge ama kwenye 
vifungashio bora. Nchini mwetu matabibu hawa wanapuuzwa.
   Hii ni pamoja na ukweli kwamba hata tiba za kisasa sehemu kubwa 
zinatokana na mitishamba ile ile wanayoifanyia uchunguzi na majaribio 
kila siku waganga wa tiba asili. Pamoja na hayo, kwa kuthamini mchango 
wa tiba asili, serikali nchini imekuwa ikiweka mikakati mbalimbali.
   Serikali ilionesha nia ya kuwa bega kwa bega na wataalamu wa tiba 
mbadala na asili baada ya kutunga mwongozo wa utekelezaji wa sera kuhusu
 tiba ya asili iliyopitishwa mwaka 2000. Mwaka 2002 Bunge la Jamhuri ya 
Muungano wa Tanzania lilipitisisha sheria namba 23 ya Tiba ya Asili na 
tiba Mbadala.
   Lakini pia serikali kuridhia uwepo wa siku ya Tiba Asili ambayo 
huadhimishwa agosti 31 ya kila mwaka ni kuonesha kuthamini mchango wa 
tiba hizi. Kwa mara ya kwanza maadhimisho ya siku hii yalifanyika mwaka 
2003 wilayani Temeke, Dar es Salaam yakilenga katika kuhamasisha 
uendelezaji na uboreshaji wa huduma ya tiba asili nchini na Afrika kwa 
ujumla.
    Chama cha Watabibu wa dawa asili nchini (ATME) mkoani Mbeya, kinasema
 serikali imekuwa na mchango mkubwa katika kuwezesha tiba asili 
kuendelea kufanyika katika mazingira stahili na yenye kulenga 
kulinufaisha taifa kwa kuwa na wananchi walio na afya njema.
  “Tunatambua jitihada zinazofanywa na Serikali kukwamua tiba asili 
nchini ili kufikia katika ubora na usalama unaokidhi vi wango kwa 
watumiaji. Imewezesha kuundwa kwa Baraza la Tiba Mbadala kwa mara ya 
kwanza mwaka 2005, kuundwa kwa miongozo mbalimbali inayolenga kuendeleza
 tiba ya Asili nchini,” anasema Mratibu msaidizi wa ATME mkoani Mbeya, 
Zahra Mansour.
   “Serikali pia imetuunganisha waganga na wakunga wa tiba ya asili 
nchini kupitia fomu zilizozinduliwa Septemba 24 mwaka 2010 na kutolewa 
kwa mujibu wa kifungu cha 14, kifungu kidogo cha kwanza cha sheria ya 
Tiba Asili na Tiba Mbadala namba 23 ya mwaka 2002, kifungu cha tatu cha 
kanuni za usajili. Hivi sasa tunao waratibu wa Tiba Asili na tiba 
Mbadala katika ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa na Wilaya,” anabainisha 
Mansour ambaye pia ni tabibu wa tiba asili.
   Pamoja na jitihada hizo zilizofanyika kwa ushirikiano baina ya 
wataalamu wa tiba, Serikali na wadau wengine bado kumekuwepo na 
changamoto mbalimbali katika eneo hilo. Changamoto hizo zinadaiwa kwamba
 zimekuwa kikwazo kwa utekelezaji wa majukumu ya wataalamu wa tiba asili
 na mbadala.
   Zipo zinazosababishwa na wataalamu wenyewe na pia zipo 
zinazosababishwa na watu wengine ama mamlaka husika. Kuwepo kwa vitendo 
vya kinyama vinavyohatarisha usalama wa watu na mali zao kutokana na 
mani za kishirikina ikiwa ni pamoja na ukiukaji wa haki za binadamu kwa 
makusudi kama vile kufanyabiashara ya viungo vya binadamu kunakoaminika 
kuhamasihwa na waganga wa kienyeji ni mambo yanayotia dosari kubwa tiba 
hizo.
   Kadhalika kushamiri kwa matangazo yasiyoendana na utaratibu wa 
sheria, miiko na maadili ya tiba asili yanayotolewa na waganga wa 
kienyeji katika maeneo mbalimbali na katika vyombo vya habari ni 
miongoni mwa changamoto hizo.
   Changamoto nyingine ni matumizi ya ramli, hasa ikizingatiwa kwamba 
ramli zinaaminika kuwa chanzo cha mfarakano katika jamii kwani imetokea 
mtu kutaka hata kumuua mama yake baada ya kudanganywa na mganga kwamba 
eti ndiye chanzo cha ugonjwa ama kifo cha mwanawe!
   Changamoto nyingine ni baadhi ya waganga kutapeli wateja kwamba 
wanatibu kila ugonjwa, kuosha nyota, kuita mpenzi, kuongeza akili za 
masomo, kuleta utajiri na mambo mengine ya kufikirika huku ukiwa ni 
uongo mtupu. Lakini Mansour anasema kwamba pamoja na yote haya, waganga 
wengi wa tiba asili wana dawa zinazotibu na wamesaidia wengi katika 
suala zima la afya.
    Hawa wanakumbana na changamoto zinazotokana na wadau mbalimbali. 
Changamoto hizo ni pamoja na baadhi ya watu kukosa uelewa na kushindwa 
kutofautisha mganga wa jadi, mganga wa tiba asili na mganga wa kienyeji.
 Anasema wataalamu hawa wanatofautiana kwa matendo, weledi wao na 
misingi ya utoaji wa huduma yao.
   Anafafanua kwamba mganga wa kienyeji mara nyingi hupiga ramli, 
wanapandisha mashetani na kutumia tunguli na wale wa jadi pia huamini 
katika mizimu, baadhi yao wakidai kwamba wamerithishwa uganga. Anasema 
waganga wa tiba asili ni watu wanaotafiti dawa, mara nyingi zikiwa ni 
dawa zilizotumiwa na mababu, waganga wa jadi na hata mpya, hawapigi 
ramli, kupandisha mashetani na mambo ya mizimu.
  Kuna uhusiano wa karibu wa tiba asili na tiba mbadala, lakini tiba 
mbadala zinachukuliwa kama tiba zisizo katika mfumo wa kihospitali 
lakini zimeshapiga hatua kubwa zaidi ya kisayansi kama vile tiba za 
matumizi ya kompyuta ama ziitwazo kwa kitalaamu kama acupuncture na 
homeopathy.
  “Ipo pia changamoto ya kuwepo kwa waganga wa kienyeji 
wanaojitambulisha kutoka nchi za nje na kufanya shughuli zao kinyume cha
 miongozo, miiko na maadili ya tiba asilia na tiba mbadala. Kutokuwepo 
pia kwa mwongozo rasmi wa rufaa za wagonjwa kutoka tiba asilia kwenda 
tiba za kisasa ni tatizo pia.
  Hatuna utaratibu wa ubadilishanaji wa taarifa, ujuzi kati ya watabibu
 wa tiba asilia na ya kisasa. “Gharama za upimaji dawa za asili 
zinazopelekwa na watabibu wa Tiba Asili katika maabara ya mkemia mkuu wa
 serikali kuona kama zinafaa kwa matumizi ya binadamu ni kubwa kiasi 
kwamba wengi kati yetu tunashindwa kumudu.
    Mtabibu wa Tiba asili na Mkunga wa Tiba Asili kudaiwa posho za kikao 
cha kujadili fomu namba moja ya mganga na fomu namba mbili ya mganga 
msaidizi zinazotolewa kwa mujibu wa kifungu cha 14 kifungu kidogo cha 
kwanza cha sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala namba 23 ya mwaka 2003 
kifungu cha tatu cha kanuni za usajili, ni tatizo pia,” anasema.
   Anasema licha ya ATME na Serikali kuhamasisha wataalamu wa tiba hiyo 
kujisajili, watabibu wengi wa tiba asilia wana mwitikio mdogo wa kuomba 
kusajiliwa, sawa na wakunga wa tiba asili.
  Zahra Mansour anasema kwamba iwapo changamoto hizo zitatafutiwa 
ufumbuzi kwa juhudi za ushirikiano wa pamoja baina ya wadau wote ni wazi
 kuwa tiba hiyo itatolewa katika mazingira mazuri zaidi na kuifanya 
jamii ya Tanzania na Afrika kwa ujumla kunufaika na tiba iliyo ya asili 
yao tofauti na ilivyo hivi sasa katika maeneo mengi.
   “Mambo ya msingi kufanyika ni pamoja na kuondolewa kwa mabango yote 
yaliyopo hivi sasa na uwekwe mwongozo wa uwekaji wa mabango mapya ya 
matangazo ya tiba za asili. Utolewe pia mwongozo wa kilimo cha miti dawa
 na uhifadhi wake ili kurahisisha pia upatikanaji wa dawa kwa uhakika.
   Tunapenda pia elimu Tiba Asili ifundishwe mashuleni kwa kuwaandaa 
wanataaluma wa tiba hiyo. Ni vema pia ofisi ya mkemia mkuu ikapewa 
ruzuku kwa ajili ya kupima dawa zetu tunazozitafiti ili kutupunguzia 
mzigo,” anapendekeza.
   Katika mkutano wa kuwakabidhi leseni za usajili wa muda watabibu 46 
wa tiba asili mkoani Mbeya, baadhi ya wadau walisema wataalamu wenyewe 
wa tiba asilia wanasababisha huduma yao kubezwa kutokana na mazingira 
wanayojiwekea, yaani kuganya kazi kwenye maeneo machafu.
    Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya, Leonard Magacha anasema mazingira 
wanamofanyika kazi baadhi ya waataalamu wa tiba asilia hayamvutii mtu 
kuyakaribia hata kama wanazo dawa mwafaka. Anasema ni vema wakatambua 
kuwa huduma wanayoitoa lazima iambatane na ubora wa mazingira kwa sababu
 wanachotibu kimsingi ni afya ya mtu ambayo inahitaji pia mashala 
pasafi.
  “Wapo baadhi ya watu wanaidharau huduma yenu kutokana na mazingira 
machafu. Badilikeni, mpende kuweka safi mazingira yenu,” anasema Magacha
 na kuongeza: “Lakini pia mmekuwa na bei ghali mno. Watu wanawaona 
matapeli kutokana na bei zenu mnazowapiga. Tatizo kidogo tu mnataka 
malipo makubwa kuliko hata mahospitalini. Sasa watu wa uwezo wa chini 
watawezaje kuja kwenu?
   Ni vizuri pia mkawa mnashauriana juu ya wale wanaowadanganya watu 
wanaoishi na VVU kuwa watawaponya kwa dawa zao. Wataalamu waliokwenda 
darasani wanashindwa kupata dawa ya Ukimwi leo mtu anaibuka eti ana dawa
 ya kuuponya. Matokeo yake inakuwa ni wagonjwa kuacha kutumia ARV na 
wanapokuja kurudi hospitali wanakuwa wameshaharibikiwa zaidi na hatimaye
 wanapoteza maisha.”
   Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Seif Mhina, 
analalamikia uwekaji holela wa mabango ya watu wanaojiita wataalamu wa 
tiba za asili. Anawataka wadau wa tiba asilia mkoani hapa kutafuta 
ufumbuzi wa kudumu wa kukomesha matangazo ya waganga matapeli 
yanayobandikwa kiholela mitaani. Mabango hayo hubandikwa katika nguzo za
 umeme, simu, miti pamoja na kuta mbalimbali.

0 comments:

Post a Comment

Mkurugenzi wa Kampuni ya Boresa na Mwenyekiti wa Jukwaa la Tiba Asili Tanzania Tabibu Boniventura Mwalongo akitoa salam za pongezi kumpongeza Mhe. DKT John Pombe Joseph Magufuli kwa Kuchaguliwa Kuwa Raisi wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo tarehe 5 Novemba 2015 katika sherehe za kuapishwa kwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli

kipanya

Popular Posts