Sunday, 28 September 2014

On 12:19 by Unknown   No comments
    AGOSTI 31 mwaka huu kulikuwa na Maadhimisho ya Siku ya Tiba Asili ya Mwafrika yaliyofanyika Zanzibar katika viwanja vya Bustani ya Victoria mjini humo.
Moja ya mambo yaliyosisitizwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Mohamed Shein, kupitia hotuba yake iliyosomwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, ni pamoja na kukemea baadhi ya watu kisiwani humo wanaojitangaza kupitia baadhi ya misikiti na mabaraza kuwa wana uwezo wa kutoa Tiba Asili, akisema kufanya hivyo ni kinyume na sheria.


Lakini pia hakusita kusema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inalipa kipaumbele suala la utafiti wa Tiba Asili na kuwa kuna uhusiano mzuri kati ya Wizara ya Afya na chama cha Watabibu Asili visiwani humo. Mwisho akaagiza mamlaka husika kushughulikia tatizo hilo.
Caroline mtafiti  wa tiba Asili kutoka chuo kikuu cha Berlin Ujerumani akipata maelezo kutoka kwa Mtabibu na Mtafiti wa Tiba Asili Bwana Boniventura Mwalongo ambaye pia ni Katibu wa ASSOCIATION OF TRADITIONA AND ALTERNATIVE MEDICINE IN EAST AFRIKA kutoka Tanzania  
Awali akisoma hotuba yake katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala Zanzibar, Mayassa Salum Ally Alisema kuwa Wizara ya Afya kupitia baraza hilo imefanya jitihada mbali mbali kuinua Tiba Asili na Tiba Mbadala na kufanikiwa kuongeza idadi ya wataalamu hao ambapo sasa kuna watabibu 193 waliosajiliwa na kuna jumla ya kliniki 18 na vilinge  125.

 Rais wa chama cha Tiba Asili na Tiba Mbadala Afrika Mashariki Lyidia Matoke Akitoa Maelezo kuhusu Tiba Asili Kwa Makamu wa Kwanza wa Rais  wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad

Sera ya Taifa ya Afya inaonyesha kuwa kabla ya Uhuru, huduma za afya zilikuwa zikitolewa zaidi katika maeneo ya shughuli za kiuchumi kama miji na mashanba makubwa. Baada ya Uhuru serikali iliweka msukumo zaidi katika kupanua huduma za afya ili kuwafikia wananchi walio wengi, hasa walioko maeneo ya vijijini.
Tiba Asili na Tiba Mbadala imekuwa ikishika kasi kila kukicha, japokuwa kuna changamoto za hapa na pale. Kuna haja ya kukubali kuwa changamoto nyingi zinazotokea katika eneo hili la Tiba Asili na Tiba Mbadala huenda zinatokana na ukosefu wa elimu ya kutosha kwa watanzania walio wengi ambao mara nyingi wamekuwa wakishindwa kutofautisha Tiba Asili na tiba nyingine zinazotolewa kwa kisingizio cha mtindo huo.
Kutokana na mkanganyiko huu, kumekuwa na tafsri za aina tofauti juu ya aina za waganga. Katika imani za kawaida, kuna aina tatu za waganga: Waganga wa Asili, Waganga wa Jadi na Waganga wa Kienyeji.
Kutokana na tafsiri inayotolewa na Chama Cha Utabibu Asili Tanzania (ATME),  Mganga wa asili ni yule anaye shughulika na tiba za maradhi kwa kutumia dawa za asili, kutibu maradhi  kwa binadamu, wanyama mimea kwa kufuata maadili ya utoaji huduma ya matibabu
Mganga wa Jadi: Anatumia Mila na Desturi katika tiba na utoaji dawa kwa wagonjwa iwe binadamu, wanyama, mimea. Hutegemea zaidi mila na desturi pamoja na tiba asili na dawa za asili kama kanuni na maadili ya utoaji huduma ya tiba.
Mganga wa kienyeji: Hana mafunzo maalumu ya tiba ya upande wowote wa tiba katika utoaji wake wa huduma kwa jamii. Ni mtu anayeweza kuchanganya taaluma mbalimbali hata za kisayansi ili mradi afanikishe alichokusudia. Mganga huyo pia anaweza kutumia vazi lolote liwe la Sheikh, Askofu, Daktari, Mganga wa Asili, ilimradi afikie lengo lake.
ATME wanasisitiza kuwa, mganga yoyote mwenye fani nzuri akiitumia katika kutenda maovu, huyo ndiye mganga wa kienyeji na wala si mtaalamu wa Tiba za Asili.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), takribani 60% ya wananchi huanza kutumia tiba asilia wanapopatwa na maradhi kabla ya kwenda vituo vya kutolea huduma za afya.
Nchini Tanzania Tiba Asili imekuwa na changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni ile ya baadhi ya watu kuihusisha na vitendo vya kishirikina, hali ambayo ni kinyume na sheria na taratibu zake, lakini pia kupotosha jamii.
Kwa mujibu wa Sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala ya mwaka 2002, watabibu wote wa Tiba Asilia na Mbadala wako chini ya Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala ambalo mbali na majukumu mengine lina jukumu la kusajili watabibu wote wenye sifa zinazotakiwa baada ya kuwafanyia usaili. Lakini pia kuendeleza na kuboresha huduma hiyo.
Moja ya mikakati ya Baraza hilo kwasasa ni kuhakikisha kuhakikisha kuwa watabibu wote wa Tiba Asili wanapata usajili, ili kudhibiti vitendo vinavyotishia maisha ya binadamu ambavyo vimekuwa vikihusishwa na Tiba Asili.
Baraza linakiri kuwa ni kweli kuwa kuna idadi kubwa ya watu anbao wanajihusisha na huduma ya tiba asili kinyemela, kitu ambacho ni kinyume na sheria. 
Katika semina ya vyombo vya habari iliyoandaliwa na ATME jijini Dar es Salaam Mei 15 mwaka huu katika Ukumbi wa NMR Dar es Salaam,  Mlezi wa chama hicho, Kingunge Ngombale Mwiru alisema Watanzania wengi ni wazito  kukubaliana na Tiba Asili, hali ambayo alisema inachangiwa na dhana ya kutawaliwa na wakoloni.
Mwenyekiti wa ATME Simba Abdulhamani Simba anasema kuna umuhimu wa serikali kuhakikisha kuwa watabibu wote wa tiba asili wanasajiliwa ili kupunguza matukio ambayo yamekuwa yakifanywa na baadhi ya watu wanaojiita wataalamu  wa tiba, lakini kwa kuichanganya na vitendo vya kishirikina.
Boninventure Mwalongo ni Mkurugenzi wa Kliniki ya Tiba Asili ya Boresa ya jijini Dar es Salaam ambaye pia ni Mratibu wa ATME, anasema kuwa kwa sasa wako katika mkakati wa kuhakikisha wanawashirikisha wadau mbalimbali ili jamii itambue umuhimu

wa tiba asili, ikiwa ni pamoja na kutoa semina kwa wadau mbalimbali.

Mwalongo anasema kuwa jambo jingine ambalo linatakiwa kudhibitiwa ni matangazo holela ya waganga ambayo yamekuwa yakibadikwa na hata mengine kutumika katika vyombo vya habari bila kufuata utaratibu.
Aidha kumekuwa na uhusiano wa karibu kati ya wadau wa Tiba Asili na Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA). Mwaka 2012 kulikuwa na mkutano wa wadau wa dawa za asili. Halikadhalika Novemba 5 mwaka jana TFDA walikutana tena na wadau wa Tiba Asili.
Moja ya malengo ya mkutano huo ilikuwa ni pamoja na kukumbushana matakwa ya sheria pamoja na changamoto za udhibiti. Katika Mkutano huoMkurugenzi Mkuu waTFDA, Hiiti Sillo alisema kuwa moja ya changamoto katika Tiba Asili na Tiba Mbadala ni kuwepo katika soko bila kufuata taratibu za utengenezaji, lakini pia akasema akaongelea juu ya baadhi ya watu kutoa matangazo katika vyombo vya habari pasipo vibali vya Mamlaka hiyo.
Mwalongo anasema kuwa mikutano kama hiyo inadhihirisha jinsi Tiba Asili inavyozidi kupata uigo na kuzidi kuthaminiwa na kwamba watanzania wanapata mwanga zaidi wa kutambua kilicho bora na kuepuka udanganyifu kwa baadhi ya watu wanaojiita watabibu asili kinyume na utaratibu.
“Kwa ushirikiano kama huu nafikiri tutafika mahala watanzania walio wengi watafahamu umuhimu wa Tiba Asili kama ilivyo katika nchi za India na China ambako kwa mujibu wa takwimu za nchi hizo asilimia 80 za raia katika nchi hizo wanategemea Tiba Asili.
Ends.

0 comments:

Post a Comment

Mkurugenzi wa Kampuni ya Boresa na Mwenyekiti wa Jukwaa la Tiba Asili Tanzania Tabibu Boniventura Mwalongo akitoa salam za pongezi kumpongeza Mhe. DKT John Pombe Joseph Magufuli kwa Kuchaguliwa Kuwa Raisi wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo tarehe 5 Novemba 2015 katika sherehe za kuapishwa kwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli

kipanya

Popular Posts