Tuesday, 28 October 2014

On 08:15 by Unknown   No comments
Tiba Asili itakavyotangazwa kimataifa
NA MWANDISHI WETU, Dar
KUANZIA Novemba 16 hadi 23 mwaka huu, kutakuwa na tukio la kihistoria katika Viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam. Kutafanyika Maonyesho ya Bias
hara ya Kimataifa ya Tiba Asili ya Mwafrika.
Maonyesho haya yanafanyika nchini kwa mara ya kwanza na yameandaliwa na Jukwaa la Tiba Asili Tanzania kushirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE).
Wadau mbalimbali wa Tiba Asili na Tiba Mbadala kutoka nje na ndani ya Bara la Afrika wanatarajiwa  kushiriki katika maonyesho hayo ambayo kauli mbiu yake ni ‘Ushirikiano wa Tiba Asili na Tiba za kisasa katika kuhimarisha huduma ya Afya Afrika’
Makundi makuu ya washiriki wa maonyesho hayo ni pamoja na Watabibu wa Tiba Asili, Watengenezaji wa Dawa Asili, Wakunga wa Tiba Asili, Kampuni za Dawa Asili na vipodozi vya dawa asili, Wasambazaji wa Tiba Asili na Tiba Mbadala, Watengenezaji wa vyakula asili, kliniki za Tiba Asili na Tiba Mbadala.
Kumekuwa na maoni mbalimbali kutoka kwa baadhi ya wadau wa Tiba Asili na Tiba Mbadala juu ya maonyesho hayo huku wengi wao wakisema kuwa yatatoa nafasi kwa wadau wa Tiba Asili na Tiba Mbadala kujitangaza kwa mapana zaidi.
Lakini pia kuna waliokwenda mbali zaidi na kusema kuwa kuna uwezekano mkubwa wa maonyesho hayo kuibua dawa nyingine za Tiba Asili kwa kujua ziko kwa nani, ni nani alifanya utafiti wa dawa hizo.
“Haya ni maonyesho ambayo yanatoa fursa pekee kwa watabibu na wadau wengine wa Tiba Asili na Tiba Mbadala kubadilishana mawazo kwa kile walicho nacho.
“Hii ina maana ya kwamba mshiriki kutoka Tanzania atajifunza jambo kutoka kwa mshiriki kutoka Uganga, Kenya na nchi nyingine zitakazoshiriki. Hii ndiyo faida mojawapo kwa wale watakaopata nafasi ya kushiriki katika maonyesho hayo,” alisema Simba A. Simba, ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Watabibu wa Dawa Asili Tanzania (ATME).
Hyasinta Ntuyeko ni muuzaji wa bidhaa za asili jijini Dar es Salaam ambaye anasema kuwa alipopata taarifa juu ya maonyesho hayo alivutiwa, akachukua fomu ya ushiriki akiwa anaamini kwamba ana kitu cha kujifunza kupitia maonyesho hayo.
 “Ni maonyesho mazuri kwasababu yatashirikisha watu kutoka nchi mbalimbali. Nafikiria kuwa hii ndiyo fursa pekee ambayo tunaweza kuitumia ikatujenga zaidi sisi wadau wa bidhaa za Tiba Asili na Tiba Mbadala,” alisema Hyasinta ambaye pia ni mtengenezaji na muuzaji wa taulo tiba za akina mama.
Innocent Oroki ni mmoja wa watengenezaji na wasambazaji wa dawa Asili kutoka Machame Moshi. Anasema kuwa anachofanya kwa sasa ni maandalizi ya dawa mbalimbali ambazo anataka watu wazione kwa wingi wakati wa maonyesho hayo.
“Kwa kuwa kupitia maonyesho haya tutapata fursa ya kuelimishana, nafikiri kwa upande wetu tumefikiria kuandaa dawa nyingi zaidi ili wenzetu kutoka nchi nyingine waweze kuziona na kutujua zaidi katika huduma hii ya Tiba Asili.
“Tiba Asili na Tiba Mbadala bado inahitaji kufahamika kwa watanzania walio wengi, Ninaamini maonyesho haya ni fursa muhimu kwetu kufanya hivyo kwa kuwapa elimu sahihi,” alisema Innocent
Lakini pia hakusita kuwakemea wale wanaotumia kofia ya tiba asili kufanya vitendo vinavyohatarisha maisha ya binadamu akidai kuwa hiyo ni moja ya changamoto kubwa ambazo bado wanahitaji kupambana nazo katika huduma ya Tiba Asili na Tiba Mbadala.  
“Changamoto nyingine kubwa tuliyonayo kwa sasa katika Tiba Asili na Tiba Mbadala ni baadhi ya watu wanaojiita watabibu wa Tiba Asili, kutumia mwavuli huo kufanya vitendo vya kuhatarisha maisha ya watu.
“Hili nalo tunahitaji kulikomesha kwa kuwaelimisha wananchi ili watambue na kufahamu mahala sahihi pa kupata huduma ya hizo kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa na serikali,” alisema Innocent, ambaye hivi karibuni alikuwa jijini Dar es Salaam akifuatilia taratibu za kushiriki katika maonyesho hayo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya maonyesho hayo Boniventure Mwalongo anasema kuwa wanatarajia washiriki 280 kutoka nje na ndani ya nchi. Lakini pia anafafanua kuwa wamekuwa katika maongezi na taasisi na kampuni mbalimbali ambazo zimeonyesha kutaka kudhamini maonyesho hayo.
“Tuna maongezi na taasisi pamoja kampuni mbalimbali. Tayari baadhi zimekubali kutudhamini. Taarifa rasmi tutaitoa pale maongezi yatakapokuwa yamekamilika,” anasena Mwalongo.
Amewataka wadau wa Tiba Asili na Tiba Mbadala kujitokeza kwa wingi akielezea kuwa baada ya hapo watakuwa na mtandao mzuri wa wadau mbalimbali wa Tiba Asili na Tiba Mbadala katika Bara la Afrika.
“Kama maonyesho haya yamebeba jina la Afrika, basi hata sisi tutahakikisha tunajenga mtandao wa wadau wa Tiba Asili na Tiba Mbadala na hasa katika suala zima la kuhimarisha soko.
Kwa mujibu wa Mwalongo, gharama za kushiriki zimegawantika katika makundi tofauti ambapo Watambuzi wa magonjwa, watengenezaji wa dawa asili, wakunga wa tiba asili, Wenye virutubisho vya tiba asili na  wauzaji wa dawa asili gharama yao ni 100,000/-. Kampuni za dawa asili na vipodozi asili zitalipa 500,000/-.
Wasambazaji wa dawa za asili na dawa mbadala watatakiwa kulipa ada ya 1,000,000/-. Wauza vyakula asili  watalipia 150,000/- wakati kliniki ya tiba asili watalipia 1,500,000/- Kliniki ya tiba mbadala gharama yake ni 2,000,000/-. Kampuni za virutubisho kutoka nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki zitalipia  dola za Marekani 1,500.
Viwango vingine ni dola 500 za Marekani kwa Kampuni za Tiba Asili ndani ya Jumuiya ya Afrika Mshariki. Gharama za ushiriki kwa Benki, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Taasisi za Serikali ni 2,000,000/-. Wajasiliamali wa kazi za uchongaji watalipia 500,000, wakati vyama vya tiba asili vitalipia 1,000,000.
Aidha Mwalongo alitoa wito kwa makundi mengine ambayo yangependa kushiriki, kujitokeza mapema ili taratibu ziweze kufuatwa. “Huenda kuna makundi mengine ambayo labda tumeyasahau, lakini milango bado iko wazi kwa yeyote ambaye angependa kushiriki maonyesho haya,” alisisitiza Mwalongo.
Alisema kuwa wana imani baada ya maonyesho hayo kutakuwa na mtandao mkubwa wa kibiashara katika huduma ya tiba asili na tiba mbadala kwa nchi za Afrika na hata nje ya Afrika. Aidha alisema kuwa wako mbioni kuyasajili rasmi maonyesho hayo ili yawe yanafanyika kila Agosti 30 pale inapoadhimishwa siku ya Tiba Asili ya Mwafrika.

0 comments:

Post a Comment

Mkurugenzi wa Kampuni ya Boresa na Mwenyekiti wa Jukwaa la Tiba Asili Tanzania Tabibu Boniventura Mwalongo akitoa salam za pongezi kumpongeza Mhe. DKT John Pombe Joseph Magufuli kwa Kuchaguliwa Kuwa Raisi wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo tarehe 5 Novemba 2015 katika sherehe za kuapishwa kwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli

kipanya

Popular Posts